• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Zuio la msajili wa vyama vya siasa kwa CHADEMA laleta mjadala na Utata

Bynijuzetz

Jul 26, 2023

Hatua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kusitisha mkutano wake kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwashirikisha viongozi wa dini, limeibua mjadala miongoni mwa wadau.


Mkutano aliotaka msajili usifanyike ni ule uliofanyika juzi katika uwanja wa Bulyaga wilayani Temeke, Dar es Salaam uliozungumzia utata wa mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji na uboreshaji bandari kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai.
Kadhalika, mkutano huo ulihusisha wadau mbalimbali wakiwemo wanasheria, wanaharakati na wanasiasa wanaotoka nje ya Chadema, viongozi wastaafu wa Serikali na viongozi wa dini.
Viongozi wa dini waliokuwepo ni Askofu William Mwamalanga na Askofu Maximillian Machumu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kibaha.
Si hao pekee waliopaswa kushiriki, viongozi wengine wa dini walioalikwa, lakini hawakuhudhuria na kwa mujibu wa Askofu Mwamalanga kutoshiriki kwao kulitokana na kutishwa.
Barua kutoka ofisi ya msajili iliyosainiwa kwa niaba yake na Sisty Nyahoza kwenda Chadema ya Julai 22, mwaka huu siku moja kabla ya mkutano huo ilikitaka chama hicho kusitisha mkutano na jana waende ofisini kwake.
Miongoni mwa sababu alizozitoa msajili ni kuwatumia watu kutoka taasisi hizo ikiwemo viongozi wa dini kwa kile watakachozungumza katika mkutano huo kuwa msimamo wa taaisi zao au hata hata wasipozungumza inaweza kuonekana taasisi zao zinaunga mkono kilichozungumzwa katika mkutano huo.
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema alipokea barua hiyo, lakini ilikuwa nje ya muda wa kazi, hivyo hawakuifanyika kazi na kuruhsu mkutano huo kuendelea.
Mnyika aliwauliza mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo iwapo viongozi hao waende kwa msajili ama la, alijibiwa wasiende naye (Mnyika) akasisitiza hawatokwenda.
Hata hivyo, mjadala uliozuka katika mitandao ya kijamii ukijikita kwenye hoja iweje Chadema iandikiwe barua ya kusitisha mkutano kwa sababu ya kushirikisha viongozi wa dini, wakati vyama vingine vinafanya hivyo bila kuzuiwa na ushahidi wa picha kutumwa mitandaoni.
Miongoni mwa picha zilizosambazwa ni ile inayomwonyesha aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum akishiriki jukwaa la siasa katika mkutano wa hadhara wa CCM.
Kutokana na hilo, Mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Hadija Mwenda alisema awali kulikuwepo na ruhusa ya viongozi wa dini kushiriki majukwaa hayo, ndiyo maana taasisi ya kuchunguza uchaguzi ya UDSM (TEMCO) ilishirikiana na viongozi wa dini katika shughuli hiyo.
“Lakini mwaka 2020, Serikali ilizuia kushirikisha viongozi wa dini kwenye hilo, kuanzia hapo hawakushirikishwa,” alisema.
Alisema hatua hiyo inaibua swali nini kiliifanya Serikali iruhusu ushiriki wa viongozi wa dini katika siasa kabla ya 2020 na baadaye ikaamua kuwazuia.
Alieleza kuwa Jaji Mutungi anaweza kujenga hoja kupitia matakwa ya Katiba kwamba Serikali haina dini, lakini hoja nyingine anaweza kuijengea kupitia sheria ya usajili wa taasisi za kidini.
“Sheria anayoisimamia ya vyama vya siasa haifanani na ile ya usajili wa taasisi za kidini, hapo anaweza kujenga hoja kwamba hawa wanaoshirikishwa si watu ninaowasimamia,” alisema.
Kwa upande wake, Mhadhiri msaidizi wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Revocatus Kabobe alisema ni kosa chama chochote kuwaalika viongozi wa dini kwenye mkutano wa kisiasa.
Kwa msingi huo, alisema Jaji Mutungi alikuwa sahihi, lakini hilo linapaswa lifanyike kwa chama chochote kitakapokiuka utaratibu huo.
“Kushirikisha viongozi wa dini kwenye mikutano ya hadhara ya kisiasa ni kuwagawa watu, kwa sababu kiongozi wa dini anapaswa kuwa katikati ili akitoa neno liume pande zote,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu uamuzi wa Chadema kutokutii barua yake, Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi alisema kwa nafasi yake anaweza ama kuchukua hatua kama msimamizi wa sheria au kutumia fursa hiyo kuielimisha Chadema na vyama vyote vya siasa kuhusu hilo.
Uwezekano huo umetokana na kile alichoeleza yeye ni msimamizi wa sheria ya vyama vya siasa, ndiye mlinzi wa vyama hivyo.
“Haya sio mapambano na hata watu wa dini wana nafasi zao za kikatiba za kushiriki kwenye masuala ya siasa, lakini tutawawekea utaratibu wao,” alieleza.
Kuhusu hatua ya Chadema kukaidi wito wake, Jaji Mutungi alisema pengine hatua hiyo imetokana na ama chama hicho kutoelewa au kimekaidi ndiyo maana ana nafasi mbili za hatua.
Alifananisha kilichofanywa na Chadema kama mtoto kwa mzazi wake, akifafanua leo atakosea kesho ukimwelimisha atakiri makosa na hatarudia.
Kuhusu viongozi wa dini kushiriki mkutano ya vyama vingine bila kudhibitiwa naye, alisema ndiyo maana analenga kutoa elimu kwa vyama vyote vya siasa kuhusu suala hilo.
Alieleza kiongozi wa dini anaposimama popote kuzungumza huchukuliwa kuwa analiwakilisha dhehebu lake, ilhali ndani yake kuna waumini wenye itikadi tofauti za kisiasa.

Leave a Reply