• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Benki ya NMB imetenga fedha jumla ya sh.bilioni 20 kuwainua vijana na wanawake mradi wa (BBT)

Bynijuzetz

Aug 4, 2023

Katika kuunga mkono juhudi za Serikali kuwainua vijana na wanawake kupitia mradi wa kuwawezesha kulima, kuvua na kufuga kibiashara (BBT), Benki ya NMB imetenga fedha jumla ya sh.bilioni 20 pamoja na kuwaelimisha vijana na wanawake hao namna ya kupata mikopo.

Pia NMB imetenga Sh.bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao ya wakulima nchi nzima ambapo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita jumla ya Sh.bilioni saba zilitolewa.

Hayo yameelezwa na Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu kusini Straton Chilongola, wakati akimweleza Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, alipotembelea banda la Benki hiyo katika viwanja vya John Mwakalange kwenye maonyesho ya sikukuu ya wakulima Nanenane 2023 jijini Mbeya yanayofanyika kimataifa.

Meneja Chilongola amesema pamoja na mambo mengine pia Benki ya NMB inatoa huduma ya mikopo ‘NMB Mshiko Fasta’ ambapo wakulima wanaweza kukopa kupitia simu za kiganjani hadi Sh. 500,000 kupitia simu za kiganja bila dhamana wala kufika kwenye matawi ya benki hiyo.

Ameeleza kuwa Benki hiyo pia ni ya kwanza nchini kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa riba nafuu ya asilimia 9 kwa mwaka na malipo ni kulingana na muda wa mazao.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa ameongozana na Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega aliipongeza NMB Banki kwa usuluhishi mbalimbali wanaoufanya kwa wakulima na namna Benki hiyo inatoa kipaumbele kwenye Sekta ya Kilimo ambayo ndio uti wa mgongo wa Taifa na kuzidi kuinua pato la Mtanzania.

Leave a Reply