• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Mbinu za Uchepushaji maji kutoka mto Ruvu zinazofanywa na wakulima wa bangi Zangundulika

Bynijuzetz

Aug 4, 2023

Operesheni iliyofanyika hivi karibuni katika wilaya tatu za Mkoa wa Morogoro imebaini uwepo wa wakulima wa bangi waliochepusha maji ya Mto Ruvu kwa ajili ya kumwagilia zao hilo.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Agosti 2, 2023 imesema operesheni hiyo iliyoendeshwa siku nane kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama iliwezesha kuteketezwa kwa ekari 489 za bangi, magunia 131 ya dawa hizo za kulevya na kilo 120 za mbegu za zao hilo.

Pia, operesheni hiyo iliwezesha kukamatwa kwa watu 18 wanaotuhumiwa kuhusika na mashamba hayo ambayo yapo katika maeneo ya kificho wilaya za Morogoro, Morogoro Vijijini na Mvomero.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alisema wakulima hao wamejiingiza katika vitendo vya uharibifu wa mazingira ili watimize azma yao ya kulima zao hilo haramu.

“Wakulima wa bangi wa mkoa huu wanachepusha maji na kuyazuia kwenda kwenye maeneo mengine ili kumwagilia mashamba yao,” alisema Lyimo.

“Wameweka mashamba huku mafichoni wakiamini hawawezi kufikiwa, ila DCEA tumewafikia na tumewakamata. Wamefanya uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kukata miti katikati ya msitu ili waweze kulima bangi, wanachofanya ni kuzidi kuharibu vyanzo vya maji katika maeneo haya na kusababisha changamoto hata kwa maeneo mengine yanayotegemea maji yatoke huku,” alisema.

Lyimo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaolima bangi na mirungi ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Novemba mosi mwaka jana wakati akifungua kongamano la kitaifa la nishati safi ya kupikia, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumzia mgawo wa maji katika Jiji la Dar es Salaam, akieleza kuwa licha ya kuchangiwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, shughuli za kibinadamu katika mto Ruvu zimechangia kupungua kwa maji.

Kutokana na tukio hilo, aliwaagiza wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kukagua katika maeneo yote yanayozunguka mto Ruvu na kuhakikisha vizuizi vyote zinavyozuia maji kuingia kwenye mto huo vimetolewa.

“Mgawo unaoendelea Dar es Salaam ni athari ya mabadiliko ya tabianchi, kwa kiasi kikubwa kupungua maji katika Mto Ruvu ni matendo yetu wenyewe binadamu. Watu wamevamia wanapeleka maji kwenye mashamba yao, nendeni mkahakikishe mto uko salama,” alisema.

Leave a Reply