• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Familia na viongozi wa dini waanza kuyazungumzia mazuri ya hayati JPM

Bynijuzetz

Aug 9, 2023

Utawala wa Magufuli ulioingia madarakani Novemba 5, 2015, ulikoma Machi 17, 2021 kufuatia kifo chake kilichotokea katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam na mwili wake kuzikwa nyumbani kwake Chato, Mkoa wa Geita.

Kutokana na kifo hicho, Samia Suluhu Hassan aliyekuwa makamu wa Rais, aliapishwa kuwa Rais Machi 19, 2021.

Waache upotoshaji

Wakati mengi yakisemwa juu ya Magufuli, Ngusa Simike, msemaji wa familia amewataka Watanzania kuacha upotoshaji kuhusu maisha ya Hayati Magufuli.

Akizungumza Agosti 5, 2023 jioni jijini Mwanza kwenye uzinduzi wa kitabu kinachoeleza historia ya Rais Magufuli, ‘Africa Magufuli and Change’ (Afrika Magufuli na mabadiliko), Ngusa alisema endapo kiongozi huyo angekuwa hai angeeleza chanzo cha uamuzi aliochukua katika uongozi wake.

Kitabu hicho kimeandikwa na Profesa Malango Chinthenga, mkurugenzi wa taaluma, tafiti na uchapishaji wa Chuo Kikuu cha Hebron (UHB) nchini Malawi.

Samike ambaye aliwahi kuhudumu Mnikulu Ofisi ya Rais, Ikulu wakati wa uongozi wa Magufuli, alisema kiongozi huyo angekuwa hai huenda angewaeleza Watanzania kwa nini alikuwa akifanya uamuzi mgumu kuhusu masuala ya nchi.

“Kifo ni mapenzi ya Mungu, yeye mwenyewe (Magufuli) angekuwa hai angepata fursa siku moja kuzungumzia legacy (urithi) yake juu ya maamuzi aliyochukua akiwa madarakani, lakini kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu aliondoka kabla hajapata hiyo fursa.

“Hiyo haimaanishi kwamba sisi ambao tuko hai tuna haki zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu na hususan kwa baadhi ya watu wanapotosha kuhusu legacy ya Magufuli. Mungu ndiyo anayepanga yote, tusipotoshe,” alisema Simike ambaye tangu kifo cha Magufuli amekuwa akizungumza kwa niaba ya familia, ikiwemo siku ya mazishi.

Samike, aliyewahi kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza na Lindi wakati wa utawala huu wa Rais Samia, alisema, “hata kama (Magufuli) hutaongea leo, ipo siku ukweli utaongea hata kama hautatoka Tanzania basi ukweli huo utaongea kutoka Malawi.”

“Kwa namna ya pekee nikiwa kama msaidizi wake, Profesa (Chinthenga) naomba nikupe zawadi kwa jinsi ulivyotafuta ukweli na kuandika kuhusu utumishi wa Hayati John Pombe Magufuli kuhusu bara la Afrika,” alisema Samike.

Alileta mageuzi

Profesa Chinthenga, mwandishi wa kitabu hicho, alisema alianza kukiandika mwaka 2017; miaka miwili tangu Rais Magufuli aingie madarakani na kuleta mageuzi katika maendeleo ya Tanzania kupitia sera ya viwanda.

Alisema kutokana na matendo ya Rais, yeye huyo aliamua kuandika kitabu kwa lengo kuonyesha jinsi Waafrika wanatakiwa kujiamini na kujisimamia katika ulinzi wa rasilimali zao badala ya kutegemea mataifa ya Ulaya kupata maendeleo.

“Magufuli alitufanya tuandike kitabu ambacho kitakachoikomboa Afrika kupitia sera na mfumo wake wa uongozi. Mfumo wa uongozi wa kiongozi huyu ulilenga kuiondoa Afrika katika ukoloni mamboleo, jambo ambalo linapaswa kuendelewwa na kila Mtanzania na Afrika kwa ujumla,” alisema.

Alisema kitabu hicho ambacho ni matokeo ya ukusanyaji wa taarifa, kuwasilisha taarifa kutoka mikoa ya Tanzania na nchi zaidi ya 23 Afrika, kinaeleza kinagaubaga namna mfumo wa uongozi wa Magufuli unavyoweza kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa mataifa ya Afrika.

“Kitabu hiki kimeandikwa kuhakikisha tunakuwa huru dhidi ya ukoloni mamboleo, kitatumiwa katika taasisi za elimu na zisizo za elimu. Kupitia humo vizazi vyetu vitajifunza kwa undani kuhusu rais huyo,” alisema.

“Hata kwenye mkutano alioalikwa Manhattan nchini Marekani hakuhudhuria ili kupata muda wa kutosha kuwatumikia wananchi wake, ndiyo maana ndani ya kitabu kuna mada inayosomeka Missing in Manhattan (kukosekana Manhattan),” alisema

Mambo saba ya Magufuli

Katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na watu mbalimbali, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Elimu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Dk Anne Gongwe alimtaja Hayati Magufuli kama kiongozi wa mfano na kuigwa barani Afrika huku akidokeza mambo saba aliyosema kiongozi huyo aliyafanya kwa mafanikio.

Aliyataja mambo hayo kuwa Magufuli alifanikiwa kuanzisha wazo la sera ya viwanda na kuitekeleza kwa vitendo kwa kufufua viwanda vilivyokuwa vimekufa na kuanzisha vipya ili kupambana na changamoto ya uzalishaji na ajira kwa vijana.

Pia, alihakiki na kuondoa wafanyakazi hewa serikalini, kuongeza usimamizi wa rasilimali za Watanzania, mapambano dhidi ya rushwa, ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na kuwaaminisha vijana kufanya na kuwa kufanya kazi kwa bidii ndiyo njia pekee ya kufanikiwa.

Awali, akifungua kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Saut, Profesa Costa Mahalu alisema uamuzi wa Profesa Chinthenga kuandika kitabu hicho ni hatua nzuri katika kuyafanya mawazo ya Rais Magufuli yaendelee kuishi.

Pamoja na kununua nakala 10 za kitabu hicho kwa Sh1.5 milioni, Profesa Mahalu aliwataka wasomi kuendelea kuenzi mazuri ya Magufuli kwa kuonyesha uzalendo wake kwenye maandishi na kuhubiri uzalendo wake kwa Watanzania.

Kwa upande wake, Kuhani wa Imani ya Rastafari Tanzania, Valeran Bagaile alisema Magufuli ni kiongozi wa kuigwa miongoni mwa wengi huku akieleza kuvutiwa na uwezo wake katika kusimamia uadilifu kwenye ofisi za umma.

Bagaile alimfananisha kiongozi huyo na alivyokuwa kiongozi wa Imani ya Rastafari, Haile Silasie ambaye aliongoza kwa lengo la kuleta ukombozi wa Afrika (Pan Africanist), hivyo kuwataka viongozi walioko madarakani kutoishia kusifia viongozi hao, badala yake watumie uzoefu wao kama chachu ya mabadiliko katika nchi zao.

“Magufuli alikuwa kiongozi wa tofauti sana, pamoja na kuwa Mkristo ila aliweza kutuunganisha watu wa imani zote katika kushiriki kwenye shughuli zinazochangia maendeleo ya umma. Hii ndiyo aina ya viongozi ambao tunatakiwa kuwa nao Afrika,” alisema.

Kilio cha uzalendo

Katika hafla hiyo, Mwanafunzi wa kidato cha sita, Sekondari ya Nganza jijini Mwanza, Florida Rugemalila alisema ukosefu wa elimu ya uzalendo kwa viongozi wa umma umechangia baadhi yao kushindwa kutekeleza wajibu wao kama alivyofanya Hayati Magufuli.

Leave a Reply