• Tue. Feb 27th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Mkono wa abiria uliosagika kwenye ajali ya basi umekatwa

Bynijuzetz

Aug 9, 2023

Abiria waliopata ajali katika Basi la Al-Saedy juzi asubuhi waliendelea na safari baada ya kutafutiwa usafiri mwingine, huku abiria aliyeumia mkono akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Kitete.

 Basi hilo linalofanya safari za Dar es Salaam na Tabora lilipinduka leo Alfajiri katika kijiji cha Nzigala, kata ya Kigwa wilayani Uyui.

Akizungumzia ajali hiyo juzi Agosti 7, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema abiria wametafutiwa usafiri isipokuwa mmoja aliyevunjika mkono ambaye amebaki kwa ajili ya matibabu.

“Abiria wametafutiwa usafiri na mmoja aliyevunjika mkono ndiye amebaki na anapata matibabu japokuwa sijui anapatiwa wapi matibabu lakini kabaki,” alisema.

Ameeleza bado wanaendelea kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kuwa wanamshikilia dereva wa basi hilo kwa mahojiano.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete Dk Reenatus Burashahu amesema kuwa walipokea majeruhi wanne ambapo watatu walitibiwa na kuruhusiwa leo mchana, huku mmoja ambaye ni mwanamke mtu mzima akikatwa mkono wake wa kushoto.

Amesema majeruhi aliyekatwa mkono aliumia baada ya mkono wake kusagika na kulazimika kuondolewa na anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.

“Mkono wake wa kushoto ulisagika kutokana na ajali hiyo na amekatwa kuanzia sehemu ya begani,” amesema.

Leave a Reply