• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Jeshi la Polisi lataja sababu za kukamatwa kwa Mwambukusi na wenzake

Bynijuzetz

Aug 15, 2023

Wakati taarifa za kukamatwa na kushikiliwa wakili Boniface Mwabukusi na wanzake wawili, zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, Jeshi la Polisi limesema halina taarifa hizo.

JUZI alfajiri taarifa zilianza kusambaa zikieleza, Mwabukusi pamoja na Katibu wa Chadema Kanda ya Kati, Emmanuel Masonga na Mdude Nyagali walikamatwa wakiwa kwenye gari moja eneo la Mikumi mkoani Morogoro. Ilielezwa walizuiwa kwenye kizuizi na watu waliojitambulisha kuwa polisi.

Hata hivyo, alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alisema hajapata taarifa za kukamatwa kwa watu hao.

Baada ya kutafutwa kuhusu suala hilo alisema hakuna aliyekamatwa na endapo atapata taarifa atazitoa.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola akizungumzia suala hilo alisema walikamatwa wakiwa Mikumi na wao wakiwa viongozi wa mkoa wamefuatilia.

Alisema walifika kituo Kikuu cha polisi Morogoro ambako waliambiwa hawapo labda wafuatilie kwingine na kwamba mkuu wa upelelezi mkoani humo (RCO) wamewasiliana naye na aliwataka wafike ofisini kwake baada ya nusu saa.

“Ni kweli wamekamatwa Mikumi na kuna kiongozi wetu pale tunawasiliana naye yuko kituo cha polisi amemuona wakili Mwabukusi na amemkabidhi ufunguo wa gari. Ameambiwa amepelekwa chumba cha upelelezi kituoni hapo hivyo anasubiri,” alisema Okola.

Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Gwamaka Mbugi alisema walielezwa baada ya kutoa maelezo wataanza safari ya kuwarudisha Mbeya wanakodaiwa walitenda makosa ya uchochezi. “Katika ufuatiliaji wetu tulibaini safari haikuwa ya Mbeya, baada ya kutoka Mikumi uelekeo ulikuwa Morogoro. Tunaendelea kuwasiliana na mawakili wa Mbeya, Morogoro na Dar es Salaam, kujua ni wapi watakuwepo,” alisema Mbugi.

Mwabukusi hivi karibuni aliwawakilisha wadai wanne katika kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kupinga mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA), akiwa kiongozi wa jopo la mawakili.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 ilifunguliwa na Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus dhidi ya Serikali.

Agosti 10, mwaka huu Mahakama ilitoa hukumu ya kuitupa kesi hiyo ikisema haina mashiko.

Juzi, Jeshi la Polisi lilionya wanaoandaa maandamano ya nchi nzima ili kuiangusha Serikali kabla ya mwaka 2025, likisema waandaaji wanayahusisha na kushawishi jumuiya ya Watanzania kuwaunga mkono katika hoja kuhusu Bandari.

Bila ya kutaja majina au kikundi cha watu, Mkuu wa jeshi hilo (IGP), Camillius Wambura akizungumza na waandishi wa habari alisema kuna taarifa zinasambaa katika mitandao ya kijamii inayohusu maandamano hayo.

Hata hivyo, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya kutoa hukumu katika kesi ya IGA, wakili Mwabukusi alitangaza uwepo wa maandamano.

Leave a Reply