• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Huduma ya CT-Scan yaanza kutolewa kwa mara ya kwanza katika Hospitali ya Sokoine-Lindi

Bynijuzetz

Aug 15, 2023

Mganga Mfawidhi, Hospitali ya Sokoine mkoani Lindi, Alexander Makalla amesema kwa mara ya kwanza hospitali hiyo ya rufaa imaeanza kutoa huduma ya CT-Scan huku wagonjwa 28 tayari wametibiwa.

Hayo ameyasema jana Jumapili Agosti 13, 2023 wakati akisoma taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo kwa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa pia ni mlezi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara.

“Mradi huu ulianza tangu mwaka 2021/2022 kwa majengo matano kwa magonjwa ya dharula, idara ya magonjwa mahututi, nyumba ya mtumishi idara ya wagonjwa wa nje na idara ya mionzi,” amesema.

“Pia tunatoa huduma za CT-Scan, usafishaji damu, endoscop na Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) ambazo zilikuwa hazipatikani zamani, sasa zinapatika kwa viwango bora zaidi na itapunguza rufaa za wagonjwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,”ameongeza.

Makalla amesema ujenzi huo umegharimu Sh7.9 bilioni na utahudumia wagonjwa 200 kwa siku.

Kwa upande wake Waziri mkuu mstaafu ambaye ni mlezi wa mikoa ya Lindi na Mtwara, Mizengo Pinda amewataka wananchi wa Mkoa wa Lindi kutoa ushirikiano kwa watumishi watakaoletwa kutoa huduma.

“Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) anatupenda sana ametuletea mradi mkubwa wa Sh7.9 bilioni kwa wakazi wa Lindi, tutoe ushirikiano kwa watumishi wetu watakaokuja kwa ajili ya kutuhudumia,” amesema Pinda.

Mkazi wa eneo hilo, Fatuma Ismail amesema kuwa anaishukuru Serikali kuwasaidia kupata hospitali kubwa ya rufaa ambapo awali baadhi ya huduma zilikuwa hazipatikani kama huduma ya mionzi.

pinda yupo mkoani Lindi kwa ziara ya siku sita kwaajili ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Leave a Reply