• Fri. Feb 23rd, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Wadau wa haki za binadamu wakemea na kulaani hatua zilizochukuliwa na Serikali juu ya Wakili Mwambukusi na Dk. Slaa

Bynijuzetz

Aug 15, 2023

Wadau wa haki za binadamu Tanzania na mashirika ya kimataifa wamelaani kitendo cha kukamatwa kwa wanasiasa na wanaharakati wanaopinga mkataba wa bandari na kampuni ya DP World ya Dubai akiwamo mwanasiasa mkogwe Tanzania, Dk Wilbroad Slaa, na kuzitaka mamlaka kuwaachia watu hao bila masharti yoyote.

Mashirika yaliyotoa tamko ni Kituo cha sheria na haki za binadamu Tanzania, LHRC, Watetezi wa haki za binadamu(THRDC), Jukwaa la Katiba(JUKATA) na Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS). Pia Shirika la utetezi wa haki za binadamu la kimataifa, Amnesty International limetoa taarifa leo na kuzitaka mamlaka za nchini hapa kuwaachia mara moja, bila masharti, Slaa, na wakili Boniface Mwabukusi, na mwanaharakati Mdude Nyagali.

Wadau hao walioungana kwa pamoja ni Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) pamoja na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).

“Kama ilivyofanyika kwa Wakili Boniface Mwabukusi na Nyagali, Dk Slaa alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi lakini baadae tuhuma zikabadilishwa na kuhojiwa tena kwa tuhuma za uhaini,” amesema Henga.

Amesema kitendo hicho ni kinyume na kanuni za kimataifa za upelelezi wa makosa ya jinai.

Akisoma tamko hilo, Henga ametoa wito kumtaka Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia kati suala hilo ili watuhumiwa waachiwe bila masharti kwani ni dhahiri kwamba hawajatenda kosa la uhaini hata kidogo kulingana na masharti ya kosa hilo.

Pia wamelitaka Jeshi la Polisi kuheshimu haki na uhuru wa kutoa maoni huku wakisisitiza mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande kuhusu mfumo wa haki jinai nchini yaheshimiwe.

“Tunatoa wito kwa wanasiasa kuachana na kutoa matamko ambayo wakati mwingine hupelekea uvunjifu wa haki za binadamu kupitia Jeshi la Polisi,” amesema Henga.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) Ananilea Nkya amesisitiza kuwa kosa la uhaini halijafanywa nchini kwa miaka mingi huku akiwataka Jeshi la Polisi kuwa makini na matamko yanayoweza kuchafua taswira ya nchi.

Leave a Reply