• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Malasusa achaguliwa kuwa Askofu mkuu mteule wa KKKT

Bynijuzetz

Aug 25, 2023

Mkutano Mkuu wa 21 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) umemchagua Askofu Alex Malasusa kuwa mkuu mteule wa KKKT.

Askofu Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani anachukua nafasi ya Askofu Fredrick Shoo aliyemaliza muda wake wa uongozo wa awamu mbili.

Anarejea tena kwenye nafasi hiyo aliyoihudumu kuanzia 2007-2015 alipomaliza na nafasi yake ikiongozwa na Askofu Shoo.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo mwenyekiti wa uchaguzi huo,Askofu Amon Mwenda,amesema kura zilizopigwa zilikuwa 241 ambapo kati ya hizo Malasusa amepata kura 167 sawa na asilimia 69.3 huku Askofu Abednego Keshomshahara akipata kura 73 sawa na asilimia 30.3

Askofu Malasusa alizaliwa tarehe 18 April, 1961 katika kijiji cha Kiwira Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya. Ni mtoto wa pili katika familia ya watoto nane ya Marehemu Mchungaji Gehaz Japhet Malasusa na Subilaga Timoth Malasusa.

Alisoma katika Shule mbalimbali za msingi kutokana na kuhama kwa wazazi.  Mwaka 1976 alihitimu shule ya msingi Bungo Morogoro na baadae kujiunga na masomo ya sekondari katika shule ya Kigurunyembe mwaka 1977. 

Baada ya masomo ya sekondari alijiunga na Chuo cha Uongozi wa Biashara na baadae alijiunga na masomo ya uhasibu.

Askofu Malasusa alifanya kazi katika mashirika mbali mbali likiwemo Shirika la Akiba la Taifa, kwa miaka minne na baadae kujiunga na masomo ya Theolojia. 

Katikati ya masomo hayo, alipata fursa ya kusoma vyuo vingine vya nje katika mpango wa kubadilishana wanafunzi na kuhitimu mwaka 1995. Masomo na mafunzo mengine aliyowahi kupata ni pamoja na usimamizi na utawala, pia mafunzo ya dini mbali mbali.

Askofu Malasusa alibarikiwa kuwa Mchungaji katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani Septemba 3, 1995.

Mwaka 1996 alifunga ndoa na Ericah Simon Nkonoki na kubarikiwa watoto watatu, Miriam, Michael na Mercy.

Pia Askofu Malasusa amefanya kazi za kikuhani Chuo Kikuu (Udsm), Usharika wa Mburahati, Usharika wa Yombo, Usharika wa Msasani na kuwa Mkuu wa jimbo la Kinondoni (sasa Kaskazini).  Pia Askofu amepata kuwa Msimamizi wa Kiroho (Chaplain) wa Seminari ndogo Kisarawe.

Askofu Malasusa amewahi kuwa Mkuu wa Kanisa kwa miaka 8 tangu 2007 hadi 2016 na Mkuu wa Chuo Kikuu Tumaini Makumira kwa kipindi chote.

Mstari wa Biblia anaoupenda ni Yohana 3:30 ‘’Basi hii furaha yangu imetimia.  Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua.’’

Leave a Reply