• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Benki ya Taifa ya Biashara imeungana na Ris wa Zanzibar kushiriki mbio fupi za hiyari

Bynijuzetz

Aug 28, 2023

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeungana na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na wadau wengine kushiriki kwenye mbio fupi zilizoambatana na matembezi ya hiyari (Wogging) zilizoandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya Zanzibar na Shirika la Kimataifa la Amref Afrika, tawi la Tanzania zikilenga kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga Zanzibar.

Kupitia tukio hilo ambalo ni sehemu ya kampeni ya ‘Uzazi na Maisha’, benki hiyo pia ilitoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 200 vitakavyotumika kwenye hospitali mbalimbali za Zanzibar ili kuboresha huduma ya afya visiwani humo.

Pamoja na kuzungumzia umuhimu wa mazoezi kiafya sambamba na kuwapongeza washiriki wa matembezi hayo, Dkt. Mwinyi, ameeleza matumaini yake kupitia kampeni hiyo, kwamba Serikali itaongeza vifaa tiba kwa vituo vya afya 28, sawa na asilimia 40.5 ya vituo vyote 69 vinavyotoa huduma za mama na mtoto Zanzibar.

Matembezi hayo yalianzia eneo la Kiembe Samaki kwa Butros Wilaya ya Magharibi B na kumalizikia viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Wateja wa Serikali – Benki ya NBC, Linley Kapya alisema mbali na mazoezi ya viungo, ushiriki wa benki hiyo ulilenga kuunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza na kuepusha vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga ambapo bado kiwango cha changamoto hiyo kipo juu.

‘’Kama ambavyo amebainisha Rais Dkt. Mwinyi, kwamba takwimu zinaonesha kuna vifo vya kina mama 134 kati ya vizazi hai 100,000 kwa mwaka na vifo 28 vya watoto wachanga kati ya vizazi hai 1,000 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017.

Hali hiyo husababishwa na changamoto za huduma duni za mama na mtoto katika hospitali na vituo vya afya zikiwemo uhaba wa wahudumu na tatizo la kukosekana kwa dawa,” amesema Kapya.

Leave a Reply