• Wed. Feb 21st, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Aliyefungwa kwa kughushi nyaraka za umiliki wa ghorofa kisha akapewa dhamana kusubiri rufaa arudishwa jela kumalizia kifungo

Bynijuzetz

Aug 29, 2023

Mtalaka aliyefungwa jela kwa kughushi umiliki wa ghorofa la wanandoa kisha akapewa dhamana kusubiri rufaa aliyokata, amerejeshwa gerezani kumalizia kifungo.

Tuwaha Samson Muze, ambaye alikuwa mtunza fedha wa kampuni ya World Wide Movers, alihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu kifungo cha miaka mitatu na nusu jela, Novemba 14, mwaka jana.

Mahakama hiyo ilimhukumu baada ya kumtia hatiani yeye na baba yake, Samson Tuwaha Muze kwa kosa la kughushi makubaliano ya umiliki wa nyumba ya ghorofa ya wanandoa, kuonyesha kwamba inamilikiwa na baba yake na kuwa alikuwa amempangisha yeye.

Pia, mahakama hiyo ilimhukumu yeye Tuwaha pekee yake kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kuwasilisha nyaraka ya uongo mahakamani katika mwenendo wa shauri la talaka baina yake na mtalaka weke Maimuna Soka.

Baada ya hukumu hiyo, Tuwaha alikata rufaa Mahakama Kuu akipinga hukumu hiyo kisha akaomba dhamana na akakubaliwa kuwa nje ya gereza kwa dhamana wakati akisubiri kusikilizwa rufaa yake.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Edwin Kakolaki Juni 23, mwaka huu ilimuondolea hatia katika shtaka la pili la kuwasilisha nyaraka ya uongo, lakini ikaendelea kumtia hatiani kwa kosa la kughushi.

Kufutia hukumu hiyo, Julai 31 mwaka huu mahakama hiyo iliamuru arejeshwe gerezani kuendelea na adhabu.

Akizungumza jana, Wakili wa Serikali Adolf Kisima alisema wakati hukumu ya rufaa inatolewa, Tuwaha hakuwepo mahakamani na hawakujua kama yuko nje kwa dhamana kwa kuwa maombi hayo yaliamuriwa na jaji mwingine.

Alisema alifahamu kuwa mfungwa huyo yuko nje baada ya mlalamikaji (mtalaka wake) kuanza kulalamika kuwa yuko nje, hivyo alifuata taratibu kuiarifu mahakama ambayo pia baada ya kujiridhisha ilitoa wito kwa pande zote kufika kotini Julai 31.

Baada ya wito huo Tuwaha pamoja na wadhamini wake walifika.

Baada ya kuelezwa sababu za wito huo, wadhamini waliomba wamuite wakili wake lakini Wakili wa Serikali alipinga akiieleza mahakama kuwa katika mazingira hayo hata wakili wake akifika hana kitu cha kuilezea mahakama.

Wakili Kisima alifafanua kwa tayari Tuwaha alishahukumiwa kukaa ndani akaomba dhamana, sasa dhamana imefutwa kwa hukumu hiyo, basi anapaswa kuendelea na adhabu yake mara moja.

Hata hivyo, mahakama iliridhia maombi ya wadhamini wake na kesi ikaahirishwa hadi saa 8 mchana ili kumsubiri huyo wakili huyo afike, huku mfungwa huyo akipumzishwa katika mahabusu ya mahakama.

Wakili wake, aliyefahamika kwa jina moja la Kalimba alipofika akaiomba mahakama isimfutie dhamana kwa madai ilikuwa ni ghafla, badala yake akaomba impe angalau wiki mbili ili ajiandae na kujiuguza zaidi kwa madai kuwa anaumwa.

Maelezo hayo yalipingwa na Wakili Kisima akisema mahakama ikikubali hilo itakuwa inaweka madaraja kwa kuwa watu wote wanaohukumiwa kwenda gerezani wanapaswa wepelekwe gerezani mara moja na hata wale wagonjwa wanatibiwa huko.

Jaji Kakolaki baada ya kusikiliza pande zote katika uamuzi wake alitupilia mbali maombi ya Wakili Kalimba akisema si tu maombi yake hayajaungwa mkono na ushahidi lakini pia na sheria.

Alisema hakuna sheria ambayo mahakama hiyo inaweza kuisimamia kumruhusu Tuwaha aendelee kufurahia uhuru nje ya gereza baada ya dhamana kukoma Juni 23, 2023 pale rufaa yake ilipotupiliwa mbali.

Tuwaha aliadhibiwa kifungo cha miaka mitatu na nusu, Novemba 14, 2022 na alitumikia adhabu hiyo kwa mwezi mmoja na siku mbili kabla ya maombi yake ya dhamana kukubaliwa Desemba 16, 2022, hivyo anatakiwa kutumikia kifungo kwa miaka mitatu, miezi minne na siku 28.

Leave a Reply