• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Amwagiwa majimoto na mke mwenza kisa wivu wa mapenzi

Bynijuzetz

Aug 29, 2023

“Nilipata hasira nilivyokuwa naonyeshwa na watu kuwa huyo ndiye mke mwenzangu, ndiyo nikachukua uamuzi wa kumwagia maji ya moto.”

Huyo ni Vumilia Kasomelo (32) mke mkubwa wa Ndagabwene Evalist (33), akieleza sababu za kumwagia maji ya moto mke mwenzake Mariam Paul (30) wakati amelala.

Vumilia ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Nyakakurugusi Kisiwa cha Kome wilayani Sengerema, alisema uamuzi huo ulitokana na wivu baada ya mke mwenzake kuhudhuria mazishi ya baba mkwe wao, ambaye hata hivyo hakutambulishwa rasmi na mume wake, bali alikuwa akisikia tetesi kwa watu.

“Sikuwahi kukutana naye wala kutambulishwa rasmi na mume wangu kwamba ana mke mwingine zaidi ya kusikia maneno kwa watu. Hata alipokuja msibani nilionyeshwa na watu kwamba ndiye mke mwenzangu,” alisema mama huyo wa watoto sita.

Akielezea tukio hilo lililotokea Agosti 27, mwaka huu; mke mdogo, Mariamu Paul alisema alitoka nyumbani kwake Kijiji cha Bukokwa kwenda katika Kijiji cha Lugata kwenye msiba wa baba mkwe wake, baada ya maziko saa 2 usiku alikwenda kulala, ndipo mke mwenzake alipomvamia na kummwagia maji ya moto na kukimbia.

“Sijui shida nini hadi animwagie maji ya moto, mimi niko kwangu na yeye yuko kwake. Tumekutana msibani kumzika baba mkwe wetu kaniunguza na maji ya moto,” alisema Mariamu aliyezaa watoto watatu na mwanaume huyo

Ofisa Mtendaji Kata ya Lugata, Rafael Jangole alisema baada ya kumhoji mtuhumiwa alikiri kufanya kosa hilo akidai ni wivu wa mapenzi baada ya kumuona mke mwenza.

“Tayari Vumilia amekabidhiwa kwa polisi katika Kituo cha Polisi Nyakaliro kwa taratibu zaidi za kisheria,” alisema Jangole

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilibrod Mtafungwa amesema hajapata taarifa juu ya tukio hilo lakini ameahidi kulifuatilia.

Alisema Mariam ameumia sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kumwagiwa maji ya moto huku mkono wake wa kushoto ukiungua zaidi.

Mume wa wanawake hao, Ndagabwene Evalis alisema tukio hili limemsikitisha na kumtia aibu kwa jamii iliyokusanyika kumstiri baba yake, Costantine Sululu.

Alisema si kweli kwamba mke mkubwa hakuwa na taarifa ya kuwa kuna mke mwenzake kwa kuwa alishampa hizo taarifa, japo hakuwahi kuwakutanisha hadi walipokutana msibani.

“Kwa tukio alilolifanya Vumilia, nilichukua jukumu la kumwadhibu lakini jamii ilinizuia na kunisihi niache, wakisema Serikali itachukua hatua stahiki, si mtu kujichukulia hatua mkoni,” alisema Ndagabwene.

Wifi ya wanawake hao, Yustina Evalist alisema mke mkubwa alijifanya anachemsha maji kwa ajili ya kupika ugali na baadaye walisikia kelele za kuomba msaada huku yeye akitoka ndani mbio akiwa ameshikilia sufuria.

Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Kome, Dk Victor Mwakyusa alisema walimpokea Mariam lakini kulingana na hali ya majeraha aliyokuwa nayo, walimpatia rufaa kwenda Hospitali teule ya Wilaya ya Sengerema

Leave a Reply