• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

Rais ashauri kupunguza kasi ya kuzaliana ili kuepukana na wimbi la ukosefu wa ajira

Bynijuzetz

Sep 6, 2023

Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi amesema nchi hiyo inapaswa kupunguza kasi ya kuzaa ili kuepuka janga. Rais al-Sisi alisema kuwa Misri inapaswa kupunguza watoto wanaozaliwa kwa mwaka hadi 400,000 kutoka zaidi ya milioni mbili ya sasa ili nchi hiyo iweze kutoa ajira na huduma za kijamii kwa ufanisi kwa raia wake.

Bw al-Sisi pia alikosoa wazo la Khaled Abdel Ghaffar, waziri wa afya na idadi ya watu wa Misri, kwamba “kuzaa watoto ni suala la uhuru kamili”. “Kuwaachia uhuru wao kwa watu ambao pengine hawajui ukubwa wa changamoto? Mwishowe, ni jamii nzima na taifa la Misri ndilo litakalolipa gharama,” al-Sisi, ambaye alikuwa akizungumza katika Kongamano la kwanza la Global kuhusu Idadi ya Watu, Afya na Maendeleo, alinukuliwa na shirika la habari la AFP.

“Lazima tupange uhuru huu la sivyo utaleta janga,” aliongeza.

Alidokeza kuwa Misri inaweza kuiga sera ya China ya mtoto mmoja, kwani China “ilifanikiwa katika sera yao ya kudhibiti idadi ya watu”.

Tangu mwaka wa 2000, idadi ya watu nchini Misri, mojawapo ya nchi zenye watu wengi zaidi barani Afrika, imeongezeka kwa milioni 40 hadi kufikia watu milioni 105, kulingana na Bw Abdel-Ghaffar. Bw al-Sisi pia alisema kuwa nchi nyingine za Kiafrika zinapaswa kuchukua hatua za kudhibiti idadi ya watu kwani bara hilo halina rasilimali za kutosha kwa idadi ya watu inayoongezeka.

Leave a Reply