• Sat. Feb 24th, 2024

Nijuzetz

Waambie Wanijue Wanitumie

TAMWA waitaja rushwa ya ngono kama kero kupelekea kukosekana kwa waandishi wa habari katika nafasi za juu za Uongozi

Bynijuzetz

Sep 27, 2023

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimesema kuwa rushwa ya ngono ni moja ya sababu inayochangia kukosekana kwa waandishi wa habari wanawake katika nafasi za juu za uongozi ndani ya vyumba vya habari.

Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Dk. Rose Reuben wakati wa semina ya siku moja iliyoandaliwa na Tamwa kwa kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT-T) kupitia mradi wa kuangazia rushwa ya ngono kwa wanahabari wanawake

Dk. Reuben alisema kutokana na vitendo vya rushwa ya ngono waandishi wa habari wanawake wanaishia katika ngazi ya kuripoti tu habari huku wachache wakipanda katika ngazi ya juu ya kuwa mwandishi mwandamizi, mhariri, mkurugenzi au meneja katika chombo cha habari.

Hata hivyo Reuben alisema kutokana na sababu hiyo Tamwa ilifanya utafiti mwaka jana uliothibitisha kuwapo kwa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono na udhalilishaji mwingine wa kijinsia katika vyombo vya habari ukiwamo wa kimwili na maneno.

Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Dk. Rose Reuben akizungumza na waandishi wa habari wanawake (hawapo katika picha) katika mafunzo ya siku moja kuhusu rushwa ya ngono kwa wanahabari wanawake.

“Utafiti huu ulionesha kwamba zaidi ya asilimia 68 ya waandishi wa habari wanawake walikuwa wameathiriwa na vitendo hivi vya rushwa ya ngono, pia ulionesha wanawake hao hawakuwa tayari kuzungumza kwa sababu hawaoni msaada mbele yao huku wengine waliona kwamba ni aibu kuzungumza masuala hayo.

“Wengine hawakuwa tayari kuzungumza kwa sababu walikuwa wanalinda kazi zao hivyo wanapambana hivyo hivyo kimjini mjini ili mradi aendelee na kazi yake, lakini wapo ambao walifukuzwa kazi na wengine waliamua kuacha kazi kutokana na kukataa kufanyiwa vitendo vya rushwa ya ngono,” alisema Dk. Reuben

Alisema katika kuhakikisha wanakomesha vitendo hivyo wamekuwa wakifanya mijadala mbalimbali na waandishi wa habari ili waweza kufahamu kuwa hilo ni kosa la jinai hivyo anapofanyiwa au kutengeneza mazingira ya kufanya hayo tayari anakuwa anakinzana na sheria na kuharibu tasnia ya habari.

“Ukatili wa kingono na kijinsia katika vyombo vya habari unaathiri hata maudhui ambayo tunayatoa kwa umma na inawezekana kwamba sisi ndio sababu ya ukatili huo kuendelea kutokana na kwamba hatuwezi kuweka wazi maudhui ambayo tunafanyiwa sisi nyuma ya pazia,” alisema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mstaafu wa Tamwa, Dk. Ananilea Nkya alisema rushwa ya ngono inaweza kukomeshwa na waandishi wa habari wanawake wenyewe kwa kuinuka na kufanya kazi kwa bidii huku wakijiwekea malengo ya kufika mbali zaidi kutaaluma.

“Ni muhimu kuhakikisha unafanya kazi kwa bidii na kuacha uzembe ukiwa kazini, weka malengo yako binafsi na uweze kuyafikia, heshimu kila mtu, andika stori nyingi hadi bosi wako kazini ashangae, ukifanya hayo heshima yako itakua kazini na rushwa ya ngono itakupitia mbali,” alisema Nkya

Mkurugenzi Mstaafu wa Tamwa, Dk. Ananilea Nkya

Naye Mchunguzi Mkuu na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, Bibie Msumi alisema nao wamefanya utafiti na kubaini uwepo wa rushwa wa ngono katika taasisi za elimu ya juu huku watu wengi waliokamatwa kwa makosa hayo ya rushwa ya ngono ni wahadhiri wa vyuo vikuu na vya kati.

“Watu wengi zaidi ambao tumewakamata kwa makosa ya ngono ni wahadhiri wa vyuo vikuu na vya kati, baadhi yao kesi zao tayari zimeshafika mahakamani zinaendelea kusikilizwa,” alisema

Baadhi ya waandishi wa habari wanawake kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Leave a Reply