MACHUNGU YA BOMOABOMOA YAHAMIA DODOMA

MACHUNGU YA BOMOABOMOA YAHAMIA DODOMA

5
0
SHARE


Wakati majengo ya Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na Wizara ya Maji yakiendelea kubomolewa Jijini Dar es Salaam kupisha
upanuzi wa barabara, vilio vilitawala hapo jana Mjini Dodoma katika bomoabomoa kwa watu waliojenga katika eneo la hifadhi ya kampuni ya Miliki ya Raslimali za Reli (Rahco) ambapo jumla ya nyumba 128 na vibanda vidogo 487 vimebomolewa katika eneo hilo.

Watu hao waliwekewa alama za X wakitakiwa kubomoa kwa hiari yao Novemba 25 mwaka jana kwa mara ya mwisho wakitakiwa kupisha eneo la hifadhi ya reli walilovamia.

Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Catherine Moshi amesema bomoabomoa hiyo ilihusisha vibanda vya stendi ya daladala ya
Jamatini, vibanda vya stendi ya mabasi ya kwenda mikoani, Ofisi za kampuni ya mabasi ya Shabiby na Abc, Mgahawa wa Cape
Town na kituo kimoja cha mafuta kilichokuwa karibu na ofisi za Shabiby.

Kuhusu stendi ya mabasi, amesema wamekubaliana na uongozi wa mkoa na manispaa kuwapa muda wa kuondoa stendi mbili za
mabasi yaendayo mkoani na ya daladala ya Jamatini.

“Wamesema kuondoa stendi sasa italeta shida kwa hiyo kuna makubaliano ambayo tumekubaliana na Mkuu wa Mkoa(DkBinilith Mahenge) wa kutoa muda wa waokuzihamisha,”amesema.

Amesema kuwa wamemaliza kazi hiyo kwa Dodoma Mjini isipokuwa maeneo ya kanisa, misikiti, makaburi na ambayo mahakama imezuia ikiwemo kituo cha mafuta kilichomo mkabala na stendi ya daladala ya Jamatini.

Moshi amesema wamebomoa nyumba kamili 128 na vibanda 487 ambazo waliziwekea alama lakini wapo wengine walioamua
kujiondoa wenyewe.

Amesema kuwa walishasaini mkataba na mkandarasi Novemba 29 mwaka huu na kwamba kabla ya kumkabidhi mkandarasi eneo
hilo ni lazima wahakikishe kuwa njia ya reli ziwe safi.

Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, John Banda amesema kuwa makubaliano na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt.
Benelith Mahenge yaliyofanyika Ijumaa hayakutekelezwa baada ya kufika katika eneo hilo Jumamosi akiwataka wafanyabiashara
hao kuondoka.

Awali wafanyabiashara hao waliomba kupewa muda wa kuhama na kuonyesha eneo jingine la kufanyia biashara baada ya
kuondolewa katika eneo hilo.

“Jumamosi Mkuu wa Mkoa alifika katika eneo hilo kuwapelekea wafanyabiashara majibu aliyoyapata baada ya kukutana na kamati yake ya ulinzi na usalama. Aliwaambia watu wa Jamatini ni vyema kila mmoja aondoe kibanda chake yeye mwenyewe,”
amesema.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY