Polisi Wampiga Risasi Mwanafunzi

Polisi Wampiga Risasi Mwanafunzi

19
0
SHARE

bastola

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari Gerezani, Shakil Sures amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kujeruhiwa kwa risasi na polisi kwenye mazingira ya kutatanisha.

Tukio hilo linadaiwa kutokea siku ya Jumatatu eneo la Fire, Upanga licha ya watu kusikia milio ya risasi, kushuhudia polisi wakipita na kumuona kijana huyo akiwa tayari kajeruhiwa, lakini hakuna mwenye maelezo sahihi kuhusu nini kilitokea hadi askari hao wakachukua hatua hiyo.

Baadhi ya watu waliokuwepo eneo la tukio Fire, Upanga siku ya Jumatatu walidai kuwaona askari waliokuwa eneo hilo wakirusha risasi, bila kujua walikuwa wakipambana na nani.

Mmoja wa mashuhuda, Athumani Simba alidai walidhani ni majibizano ya risasi kati ya askari na majambazi, baada ya kuona gari la polisi likipita eneo hilo.

“Niliwaona askari wawili wakielekea eneo la Fire huku wakipiga risasi, ghafla nilimuona mwanafunzi akilia huku akiwa ameshika mguu wake akiomba msaada,” alisema Simba.

Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha amesema mwanafunzi huyo alifikishwa hospitalini hapo jioni ya Jumatatu na kwamba jeraha lake linaendelea vizuri.

“Tumempokea mwanafunzi Shakil juzi jioni na kidonda chake kimesafishwa na kinaendelea vizuri,” amesema Aligaesha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Hamduni Salum amesema upelelezi kuhusu tukio hilo unaendelea. Hata hivyo, hakueleza mazingira ya tukio lenyewe yalivyokuwa.

“Tunawashikilia askari polisi wawili waliokuwa zamu siku hiyo ya tukio, upelelezi unaendelea ili kuangalia kwa nini walitumia nguvu kubwa kiasi hicho,” amesema Kamanda Salum.

NO COMMENTS

LEAVE A REPLY